KILIMO BORA CHA VIAZI LISHE

 

KILIMO BORA CHA VIAZI LISHE{VIAZI KAROTI}


✍🏿MUANDISHI:ABUU HAARITHA RAJAB🇹🇿

📝Viazi Karoti ni Viazi ambavyo ndani vina rangi ya njano au Karoti.

*AINA ZA VIAZI LISHE*

🥕Kuna Aina Nyingi za Viazi lishe ikiwemo Kabode,Mataya,Jeweli,Naspoti,Kiegea,676,Ejumla,Alveria,Mayai,Kizimbani Mayai,Kibakuli,UKG 05,Kakamega na Mlezi.

🥕Viazi hivi vina wingi wa viini lishe vya Vitamini A,Viazi hivi ni vizuri kwa chakula na Afya kutokana na kuwa na uwingi wa viini Lishe viitwavyo _beta carotene_.

*UZALISHAJI WA MBEGU ZA VIAZI LISHE*

Kuna njia Tatu za kuzalisha mbegu.
❶Uzalishaji mbegu kwa kutumia mizizi au Viazi
❷Uzalishaji wa mbegu kwa kutumia kitalu
❸Uzalishaji wa mbegu kwa kutumia Kitalu.

*UZALISHAJI WA MBEGU KWA KUTUMIA MIZIZI*
📝Mizizi hutumika kuandaa mbegu na ni Teknolojia rahisi iitwayo S tatu{Triple S,Sand,Storage and Sprouting},Wakati wa kiangazi Viazi huhifadhiwa kwenye mchanga na kumwagiliwa maji kabla ya mvua kuanza,hivyo huchipua na kutoa mbegu kabla ya mvua kuanza kunyesha.
Vifaa vinavyohitajika ni Beseni,maboksi ya kawaida,mchanga na Viazi vidogo vidogo kutoka kwenye mmea ambao hauna magonjwa na wadudu.

Weka Viazi ndani ya Udongo wakati huo upande wa mizizi uwe chini kisha endelea kumwagilia maji baada ya muda machipukizi yatatoka utandelea kumwagilia maji na kuzitunza mpaka utakapoanza kuvunwa mbegu.
Teknolojia hii hutumika hasa kwenye maeneo yenye mvua kidogo au sehemu zenye muda mrefu wa ukame.

*UZALISHAJI WA MBEGU KWA KUTUMIA KITALU AU JARUBA*

📝Njia hii ya Vitalu hutumika kuzalisha mbegu kwa haraka ziadi{Rapid multiplication}.
▪Vitalu au Jaruba tambarare vinatakiwa viwe na Urefu wa mita 6 na upana wa mita 1.2 au sentimita 120 na huandaliwa kwa kuinuliwa juu kwenye sehemu zenye mvua nyingi au maji mengi ili mbegu zisizame na kwa sehemu zenye mvua kidogo au kame kitalu kinatakiwa kilazwe chini{Sunken seedbeds} ili kuweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu.
Kwenye kitalu mbegu hupandwa kwa kipimo cha sm 10 mmea hadi mmea na mstari hadi mstari sm 20.Kwa wastani kila mita 1 ya mraba huchukua Mbegu au Vipando 50 na kila Kitalu vipando 300.
📚Katika Kitalu Unaweza kutumia mbegu au vipando vyenye urefu wa sm 15 kupandikiza.

*Uwekali wa Mbolea*
❗Weka Mbolea ya NPK yenye namba kubwa mwanzoni kwenye Kitalu mfano 20:10:10 na huwekwa kwa kiwango cha gramu 50 kwa kila mita 1 ya mraba.
❗Kama umepanda aina nyingi za mbegu kwenye Kitalu ni Vema ukaweka alama inayoonyesha aiana ya Mbegu na Tarehe ya kupanda.

UZALISHAJI WA MBEGU KWA KUTUMIA MATUTA*

Matuta huandaliwa kwa kuinuliwa Udongo juu kimo cha sm 90 au futi 3 na umbali wa tuta hadi tuta ni sm 90-100.
Mbegu au Rando lenye urefu wa sm 25-30 hupandwa juu ya tuta kwa kulaza na kufukia Theluthi mbili{2/3} umbali wa wa Rando moja hadi lingine ni sm 25-30.
Matuta yanaweza kutengenezwa mapana na ukapanda Mbegu mistari 2-5 au ukatengeneza tuta dogo ambalo sio pana na ukapanda mstari mmoja tu katika tuta.
Kwa Matuta makubwa ,mistari miwili kwa kila tuta wastani wa mimea ni 35,000-38,000 kwa hektari{Ekari 2.5} na Matuta madogo,mstari mmoja Kati Kati ya Tuta wastani wa mimea 33,000 kwa Hektari sawa na Vipando 13,200 kwa Ekari 1.

*UMWAGILIAJI NA PALIZI*

Unyevu wa kutosha huhitajika  kipindi kisichopungua siku 60 baada ya kupanda,mwagilia maji ya kutosha kama udongo ukiwa mkavu baada ya kupanda mpaka mizizi itakapo shika.

Palizi ni muhimu kabla ya mbegu kuenea katika shamba.Magugu katika hatua ya awali ya ukuaji huathiri ubora wa Mbegu na mavuno.

*UVUNAJI WA MBEGU*

Mbegu hukomaa na kwa tayari kwa kuvunwa kama Mbegu miezi 2-3 baada ya kupanda.
Mara Mbegu inapokomaa kata marando sm 5 kutoka Ardhini ili kuruhusu uchipuaji wa mashina au Mbegu zingine.Uvuanji mwingine ufanyike kila baada ya miezi 2-3 baada ya mvuno wa mwisho.
Inashauriwa uvunaji wa mbegu kwenye Vitalu ufanyike Mara 3{inategemea na ubora wa Mbegu/mimea},baada ya hapo utaondoa mimea yote na kuanza kupanda Upya

*SIFA ZA MBEGU NZURI/BORA ZA VIAZI LISHE*

Mbegu nzuri ni zile zenye urefu wa sentimita 25-30{inch 10-12}na majani 7-8 .Mbegu mbaya inarefuka ovyo kutokana na ukosefu wa jua{rangi ya majani na majani yenyewe ni mepesi} au mbegu ambayo ni fupi kabisa uzalishaji wake utakuwa sio mzuri na rangi ya majani mazito sana.
Mbegu isiwe na dalili za magonjwa.
Mbegu zisiwe na mashambulizi ya wadudu mfano fukusi.
Mbegu iwe na Afya nzuri
Mbegu ichukuliwe kutoka kwenye ncha kwani sehemu hii inauwezo wa kuchipua mapema na pia haitunzi mayai ya wadudu.

*MAANDALIZI YA SHAMBA*
Andaa eneo lenye udongo mzuri wenye rutuba safisha,katua na tengeneza Matuta yenye upana wa  wastani wa mita moja kutoka tuta hadi tuta na urefu inategemea na mahitaji ya mkulima.
Nafasi kati ya mmea na mmea huchangia ukubwa wa Viazi wakati wa mavuno.uchaguzi wa aina na ukubwa wa matuta inategemea na maamuzi ya wakulima mwenyewe,mazingira na mahali shamba litakapolimwa.

*JINSI YA KUPANDA*

Kuna njia mbili za kupanda Viazi Ambazo ni Upandaji wa kusimamisha na kulaza mbegu.

*UPANDAJI WA WIMA{KUSIMAMISHA}*
▪Kwa Upandaji huu wa wima idadi ya Viazi inakuwa ndogo lakini Viazi vyake vikubwa.
▪Mizizi ambayo itakuwa Viazi baadae inachipuka kutoka kiunga cha shina na majani ambayo yalikaa uso wa Udongo.

UPANDAJI WA USAWA{KULAZA}*
▪Upandaji wa mbegu kwa kulaza viungo vya majani vinakuwa vingi, Idadi ya Viazi vinakuwa vingi lakini vidogo vidogo.

*KUPANDISHA MBEGU*

Mashina ya viazi yakienea shambani kamata mashina na kuyapandisha juu ya Tuta.Baada ya kupandisha rudisha mashina kama yalivyo,lengo ni kuzuia maranda kujishikiza chini na kuota mizizi kwani uotaji wa Mizizi hupunguza nguvu za mimea na matokeo yake Viazi vyote vitakuwa vidogo vidogo.

*MAGONJWA NA WADUDU*

MAGONJWA
Kuna magonjwa mengi yanayoshambulia Viazi yakiwemo Batobato ya Viazi unaosababishwa na Wadudu mafuta pamoja na Inzi weupe,Ugonjwa wa chule{Anthracnose},na Ugonjwa wa Uozo mweusi{Black rot}.

KUDHIBITI
Panda mbegu bora, Kilimo cha mzunguko,kufuata kanuni bora za kilimo,Kutumia viua sumu kwa magonjwa yanayosababishwa na wadudu.

*WADUDU WAHARIBIFU WA VIAZI*
Uharibifu unaofanywa na wadudu unaeza kutokea kwenye majani,mashina au mizizi kwa kula,utobolewa au kufyonzwa
Wadudu waharibifu wa Viazi ni Fukusi mweusi,Funza wa vipepeo,Vuwavi jeshi,pamoja na wanyama waharibifu kama vile Panya Fuko.

*PANYA FUKO*

Panya fuko ni wanyama jamii ya panya amabao muda mwingi wanaishi Ardhini.
Wanyama hawa hula mizizi na kusababisha mmea mzima kunyauka na hatimae hufa.

Dalili za uwepo wa Panya Fuko.
📝Kuwepo kwa Udongo laini uliojirundika kama vichuguu,hii hutokana na Panya kuchimba na kutoa  Udongo nje ya shimo.

*JINSI YA KUDHIBITI PANYA FUKO*

❶Kuharibu mashimo ya Panya Fuko.
❷Safisha Shamba na mazingira yake.
❸Chimba mifereji yenye kina kirefu kuzunguka Shamba
❹Panda mimea yenye sumu ambayo ina mizizi mirefu kam vile _Tephrosia vogelli_
❺Panda Ufuta kuzunguka Shamba lote kwani mizizi yake ni sumu kwa Panya Fuko.
❻Mwagia maji ya moto kwenye Mashimo ili kuwababua na au Mwagia pilipili zilizotwangwa kwenye Mashimo.
❼Tega mitego katika maeneo yote
❽Weka sumu kwenye Mashimo ya Panya Fuko.

*MAVUNO*

Viazi huwa tayari kuvunwa miezi minne tangu kupanda.

Mambo ya kuzingatia katika Uvunaji wa Viazi.

❶Ondoa majani ya mashina kutoka tuta kabla ya kuvuna Viazi Vitamu
❷Weka nafasi ya kutosha kutoka Viazi mpaka sehemu ya kuchimba ili kutokuharibu Viazi kisha vuna Viazi kwa uangalifu.
❸Ondoa Viazi vitamu vilivyoharibiwa na wadudu pamoja na wanyama waharibifu,chimba Viazi kwa makini ili visichubuke ngozi yake.
❹Weka Viazi kwenye Kreti kwaajili ya kuhifadhia na kusafirisha.

♻Kwa wastani mavuno huwa ni Tani 10-30 kwa Hektari

*MAKADIRIO YA MAVUNO YA VIAZI LISHE SHAMBANI*

📝Ni vizuri kukadiria mavuno yako kabla ya kuanza uvunaji wa Viazi lishe.Unachotakiwa kufanya ni:⤵
❶Kuchimba mimea 10 bila mpangilio{Randomly}.
❷Kisha Pima uzito wa viazi kwa kila shina
❸Chukua takwimu za uzito wa viazi wa kila shina.
♻Mfano Mmea/{Uzito kwa kilo} 1{kilo 1.8}, 2{kilo 2.5}, 3{kilo 1.7}, 4{2.7},5{kilo 1.9} 6{kilo 2.1 } 7{kilo 2.6}, 8{kilo 3.3},9{kilo 1.8}, 10{kilo 2.6}
♻Tafuta wastani wa uzito wa viazi kwa Kujumlisha uzito wote ulio chukua takwimu na kisha Gawanya kwa idadi ya mimea uliyochimba.
Mfano: kilo 23÷ 10 =kilo 2.3 ambao ni wastani wa uzito wa kila mmea.Kisha Hesabu mimea yote iliyopo shambani na Zidisha jumla ya idadi ya mimea yote shambani kwa wastani wa uzito wa kila mmea
{mfano: una mimea 6,000 ya viazi shambani utazidisha kwa kilo 2.3x 6,000. Makadirio
ya mavuno yatakuwa kilo  za viazi 13800

📝Viazi ni moja ya zao linaloharibika mapema baada ya kuvuna kutokana na sababu zifuatazo⤵
❶Viazi vina kiasi kikubwa cha maji (60-70%)
❷Vina sukari (4-15%)
❸Uwezo mkubwa wa kupoteza maji
❹Ngozi laini

📝Kama nilivosema Viazi lishe vinakuwa tayari kuvuna kuanzia miezi 3 – 6 baada ya kupanda inategemeana na aina
ya viazi na ukuaji wake, mazingira{hali ya hewa, udongo, upatikanaji wa maji} na masoko.

📝Uvunaji utategemea maamuzi ya mkulima kwa muda atakapoamua kutegemea na uhitaji
📝Wengi wanatumia uvunaji wa kidogo kidogo kwa kuchagua vilivyo tayari na kuacha vingine
vikue kwenye udongo.

*NJIA ZA UVUNAJI WA VIAZI LISHE*

📝Kuna njia nyingi za uvunaji wa Viazi lishe ikiwemo njia ya mikono kwa kutumia vijiti, panga au jembe.Viazi vinaweza kuvunwa kwa kutumia trekta au jembe la kukokotwa na ng’ombe.
📝Kuna aina mbili za Uvunaji wa Viazi Lishe ambazo ni uvunaji wa kidogo kidogo na Uvunaji wa Moja kwa moja.

*1⃣UVUNAJI KIDOGO KIDOGO{PIECE MEAL HARVESTING}*
✍🏿Katika aina hii ya Uvunaji Viazi vinatakiwa vivunwe kwa makini ili kuzuia kuvijeruhi.
📝Uvunaji wa kidogo kidogo {piece meal harvesting}.Viazi huvunwa baada ya kukomaa wakulima wengi huangalia mipasuko ya udongo kwenye matuta
📝Vuna viazi vikubwa na kuacha vile vidogo ili viendelee kukua.Baada ya uvunaji hakikisha unaziba mipasuko yote ili viazi vinavyobaki visishambuliwe na wadudu chonga{weevils}.

*UVUNAJI WA SHAMBA ZIMA KWA PAMOJA*

📝Kwa uvunaji wa shamba lote huhusisha jembe la mkono,Jembe la kukokotwa na Ng'ombe Dume pamoja na Tractor.
🔝Kwa uvunaji wa kutimia jembe Anzia pembeni kuja katikati, hii inasaidia kuepuka kuvijeruhi viazi na kuvifanya viazi vioze haraka
⚡Wakati wa kuvuna, viazi vitengwe katika madaraja Viazi Vinavyouzika na visivyouzika,Vile vile Viazi vidogo sana na mashina yaliyokwisha vunwa vinaweza kuwa chakula cha mifugo au chanzo cha mbegu msimu ujao.
📝Baada y kuvuna Viazi vinatakiwa kusafirishwa kutoka shambani kwenda sokoni au kwaajili kuhifadhi.Viazi visafirishwe kwa kutumia Kreti za plastiki au za mbao.

*UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU BAADA YA KUVUNA*

📝Wadudu na magonjwa yanaweza kujitokeza baada ya kuvuna kama vile magonjwa ya kuoza yanayosababishwa na fungusi na wadudu waharibifu kama dumuzi na bungua.

✍🏿Ili kudhibiti Fanya mambo yafuatayo⤵
❶Kuepuka kupanda viazi maeneo yenye historia ya magonjwa na wadudu hao.
❷Panda mbegu bora zisizokuwa na magonjwa na wadudu
❸Usafi wa maghala
❹Zingatia kanuni za uvunaji.

*UHIFADHI NA USINDIKAJI WA VIAZI LISHE*

*UHIFADHI VIAZI*

📝Baada ya viazi kuvunwa na kuwekwa katika madaraja vinaweza kuhifadhiwa kwaajili ya matumizi ya baadae,Viazi vikihifadhiwa vizuri vina uwezo wa kukaa miezi 3-5 bila kuharibika.
🔝Viazi vibichi vinahifadhiwa kwa  kuvichimbia chini pamoja na  kujenga kivuli.

*FAIDA ZA KUHIFADHI VIAZI*

❶Mara baada ya viazi kukomaa na kuvunwa, ardhi itakuwa na nafasi ya kupanda mazao mengine
❷Kupata soko zuri lenye faida kwa kuuza viazi muda ambao sio msimu wa viazi vibichi
❸Inasaidia kuwa na uhakika wa chakula katika kaya wakati ambao sio msimu wa Viazi.

*HASARA ZA KUHIFADHI VIAZI*

❶Upotevu wa maji na uzito wakati wa kuhifadhi unaopelekea kuharibu radha na muonekano
❷Upotevu unaoweza kusababishwa na magonjwa
❸Upotevu unaosababishwa kwa kuliwa na wadudu kwa mfano bungua na wanyama waharibifu kama panya.

*UCHAGUZI WA VIAZI LISHE KWAAJILI YA KUHIFADHI*

📝Wakati wa uchaguzi was Viazi lishe kwaajili ya kuhifadhi unatakiwa kizingatia mambo yafuatayo:

❶Hakikisha unavuna Viazi kwa uangalifu na kwa wakati muafaka.
❷Hifadhi sehemu iliyoandaliwa vizuri
❸Uchaguzi wa viazi ufanyike kwa makini ili kuepuka uharibifu wakati wa kuhifadhi.
❹Chagua viazi ambavyo havijapata majeraha yoyote
❺Viazi vihifadhiwe mara tu baada ya kuvunwa.Vile vyote vinavyoonyesha dalili ya wadudu au magonjwa visihifadhiwe.

*NJIA MBALIMBALI ZA KUHIFADHI VIAZI LISHE*

📝 Kuna Njia mbili za kuhifadhi Viazi Lishe vibichi baada ya Kuvuna.

*1⃣KUHIFADHI KWENYE SHIMO*

⚡Chagua eneo chini ya kivuli
⚡Shimo liwe na ukubwa wa kutosha, lenye kina cha sentimita 70-90 na upana wa sentimita 70-90
⚡Shimo lichimbwe sehemu kavu na litandikwe majani makavu chini ikifuatiwa na mchanga mkavu ili kuzuia unyevu utakaosababisha viazi kuharibika
⚡Panga viazi jaza kama kiasi cha kilo 50-100 za viazi vibichi ndani ya shimo.
⚡Weka bomba katikati ya shimo ili hewa ya ndani iweze kutoka.
⚡Hakikisha kuwa viazi vyote unavyopanga ni vile visivyo na majeraha yoyote, michubuko au vilivyokatwa.
⚡Funika viazi kwa mchanga mkavu wenye kina sentimita 10 – 20 unene
⚡Hakikisha hakuna uharibifu wa wanyama kama panya kwa kufanya usafi wa mazingira yanayozunguka shimo.
⚡Mwisho jenga kibanda cha nyasi chenye paa juu ili kuweka kivuli kuzuia jua na mvua zisilete uharibifu au kusababisha kuoza
⚡Tengeneza mtaro wa kutoa maji kuzunguka eneo la hifadhi.

*2⃣KUHIFADHI KWENYE MATUTA{UDONGO ULIORUNDIKWA KAMA KICHUGUU}*

⚡Rundika udongo mfano wa kichuguu chenye urefu wa sentimita 10 na upana wa mita 1.
⚡Panga viazi kilo 50– 100 kuanzia katikati kuelekea pembeni
⚡Funika viazi kwa udongo kwa kina cha sentimita 10 – 20
⚡Tengeneza paa kwa kutumia matawi au majani makavu ili kuzuia mvua na wanyama.
⚡Tengeneza mtaro wa kutoa maji kuzunguka eneo la hifadhi.

📚Kwa kutumia hifadhi zote mbili viazi vinaweza kuhifadhiwa hadi miezi 4-5 wakati wa kiangazi bila kuharibika
▪Ukaguzi wa mara kwa mara wa sehemu ya kuhifadhia angalau mara 1-2 kwa wiki.
▪Kama kuna matatizo yoyote ambayo yanaoneka kuharibu viazi vyako jaribu kuyatatua, mfano wadudu,kuoza na wanyama waharibifu
▪Kama maendeleo ni mazuri endelea kuziba nafasi zilizowazi na kuongeza kivuli zaidi.

*USINDIKAJI WA VIAZI LISHE*

📝Usindikaji ni kile kitendo cha kulibadilisha zao kutoka uhalisia wake na kuwa katika sura au muonekano mwingine.
🔝Tunasindika ili kurefusha uhifadhi kwa kupunguza kiasi kikubwa cha maji kilichopo kwenye kiazi. Pia ili kuongeza thamani ya viazi, badala ya kuuza vibichi kwa bei ya chini,kwa mfano unga unauzwa kwa bei ya juu ukilinganisha na bei ya viazi vibichi, pia unaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali baada ya kusindika zao lako.
▪Usindikaji unarahisisha ukaukaji na usafirishaji hadi kufika sehemu ya masoko.

*NJIA ZA USINDIKAJI WA VIAZI LISHE*

📝Kuna njia mbalimbali za usindikaji wa viazi viazi Lishe ni njia za asili na ulioboreshwa.

*NJIA ZA ASILI{TRADITIONAL PROCESSING}*

🅰 *MICHEMBE*

📝Hatua za kutengeneza Michembe:

❶ Viazi hunyaushwa juani kwa muda wa siku 1-2 ili kupunguza maji ya ziada,kurahisisha umenyaji na ukataji wa vipande vyembamba.
❷Baada ya viazi kunyauka humenywa kwa kutumia kisu. Sehemu zote zilizoharibika wakati wa kuvuna au zilizoshambuliwa na wadudu zinaondolewa.
❸Viazi huchongwa katika vipande vidogo vidogo kurahisisha ukaukaji.Kutokana na utumiaji wa kisu katika ukataji,vipande vya viazi huwa havilingani hivyo havikauki kwa pamoja.
❹Vipande hukaushwa juani kwa muda wa siku tatu 3-4. Michembe inatakiwa ikauke
kikamilifu ilikuzuia uharibifu wakati wa kuhifadhi.
♻Pia uangalifu wakati wa kukausha/kuanika ni muhimu ili kuepuka mchanga, vumbi na uchafu mwingine.

*🅱MATOBORWA*

📝Hatua za kutengeneza Matoborwa:

❶Viazi hunyaushwa juani kwa muda wa siku1-2 ili kupunguza utomvu na kuboresha ladha.
❷Viazi husafishwa kwa maji safi kisha sehemu mbovu huondolewa.
❸Viazi vilivyosafishwa huchemshwa kwenye vyombo vikubwa kwa mfano sufuria kwa dakika 30-40.
❹Viazi vilivyochemshwa humenywa kwa kutumia mikono kwani ngozi ya kiazi hulainika na kumenyeka kirahisi.
❺Viazi vilivyochemshwa na kumenywa hukatwakatwa vipande vyembamba ili kurahisisha ukaukaji.
❻Vipande vilivyokatwa hukaushwa kwenye vichanja ili visichafuke kwenye ukaushaji juani vipande hukauka baada ya siku 3-4.

📚Kwa Njia hii ya Asili ya Usindikaji kama Usindikaji utafanyika vizuri Viazi vilivyosindikwa vitaweza kukaa kwa muda miezi 6 bila kuharibika na huhifadhiwa kwenye magunia na kisha huwekwa kwenye maghala imara linaloingiza hewa vizuri lakini pia Vinaweza kuhifadhiwa kwenye Vihenge au mapipa.

*USINDIKAJI ULIOBORESHWA*

📝Njia hizi ni ubora zaidi kwani huhusisha mashine za mkono na zile za ktumia mota ambazo hurahisisha kazi kuliko kukatakata kwa mikono.
🔝Njia hizi huzingatia kutopoteza ubora,usafi,ukaukaji wa haraka,na urahisi wa kuingia kwenye masoko.

♻Mashine inayoendeshwa kwa mota inacharanga viazi vingi zaidi kuliko mashine za mkono za kucharanga viazi.
♻Hatua za kucharanga viazi⤵
⚡Vuna viazi vilivyokomaa,vinyaushwe kwa muda wa siku 1-2,
⚡Menya, osha na vicharange katika vipande vidogo kwa kutumia mashine.
⚡Sambaza vipande vyako katika sehemu safi au kichanja halafu acha kwenye jua mpaka vikauke.
⚡Muda wa kukausha ni siku tatu

🥕Viazi lishe vilivyoanikwa kwenye kichanja Vikikauka unaweza kuvihifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadae au saga katika mashine kupata unga kwa matumizi ya mbalimbali ya vitafunwa na mengineyo kama kupikia uji.
                   ⭕✍🏿⭕
🥕Ili kuhifadhi Vitamini A{beta carotene} isipotee wakati wa kuhifadhi na usindikaji fanya mambo yafuatayo:

🥕Usisindike Viazi kwa  muda mrefu kwenye joto kubwa, usichemshe muda mrefu au usitumie mvuke kwa muda mrefu au kuchoma na kukausha kwa muda mrefu
🥕Pika Viazi na maganda yake,kuacha maganda kwenye viazi  kunafanya vitamin A {beta-carotene} iendelee kuwepo kwenye Kiazi.




*

Maoni

Machapisho Maarufu