KILIMO BORA CHA MPUNGA

 


KILIMO BORA CHA MPUNGA/RICE{ORYZA SATIVA}

UTANGULIZI:

🌾Mpunga ni zao ambalo lipo katika kundi la Nafaka na ni zao la pili la chakula kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi nchini Tanzania. 

🌾Mvua ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga.Viwango vya mahitaji ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga. Ni kwa jinsi hii

mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali kutegemea na mahitaji yake ya maji. 

 ZIPO AINA KUU TATU  ZA MAZINGIRA

Mazingira haya ni:

↪️kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea mvua

↪️kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko 

↪️kilimo cha mpunga cha umwagiliaji 

🌾Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania:Ifakara, Dakawa, Kyela, Mbarali,Kahama na Bonde la Ruvu mkoani Pwani. na maeneo mengine mengi.

UDONGO 

↪️Udongo una rutuba ya asili yaani virutubisho katika udongo, mboji {organic matter}, na viumbe mbalimbali vinavyoishi kwenye udongo. 

↪️Makundi ya udongo

Kuna makundi makuu matatu ya udongo, kutokana na ukubwa wa 

chengachenga za udongo:

▪️Kichanga {Sand soil}

↪️ Udongo wa kichanga una uwezo mdogo wa kuhifadhi maji na 

 unyevunyevu.Hivyo hukauka upesi.

▪️ Tifutifu {Loam soil}

↪️Udongo huu unahifadhi maji vizuri na upatikanaji wa maji na

 virutubisho kwa mimea ni mkubwa. 

▪️Mfinyanzi{Clay soil}

↪️ Udongo huu  unahifahdi maji mengi zaidi lakini upatikanaji wa virutubisho kwa mimea ni mdogo.


pH ya udongo (Soil pH)

↪️pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali {ph ndogo kuliko 7}, nyongo {ph kubwa kuliko 7}, au katikati {neutral} - ph ya 7.

Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita.

🌾Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani {kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0}. Mpunga

hustawi kwenye udongo wa mfinyanzi wenye tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha.

 KANUNI BORA  ZA  KILIMO CHA  MPUNGA

🌾Kuandaa Shamba Mapema

🌾Matumizi ya mbegu bora

🌾Kupanda kwa nafasi

🌾Matumizi ya mbolea

🌾Kupapalilia kwa wakati

🌾Kuzuia wadudu na wagonjwa

🌾Kuvuna kwa wakati na kuhifadhi.

KUANDAA SHAMBA MAPEMA

🌾kusafisha shamba-Wakulima wanapaswa kusafisha shamba mapema kwa kutumia majembe ya mkono,mapanga,shoka,reki nk

🌾Kulima na kulainisha udongo- ardhi inatakiwa itifuliwe kwa kutumia majembe ya mkono,trekta, power tiller,au maksai(ng’ombe) kabla ya mvua au mwanzoni wa mvua kabla ya udongo haujawa laini sana, baada ya kutifua shamba lainisha udongo kwa kuvuruka ili uwe tope kwa maeneo ya umwagiliaji kurahisha upandaji

🌾Kusawazisha udongo- ni muhimu kusawazisha udongo ktk aina zote mbili za kilimo cha mvua na umwagiliaji ili kurahisisha usambaaji wa maji na mbolea kwa jembe la mkono au mbao maalumu

🌾Kutengeneza kingo- kutengeza kingo ni  muhimu kwaajili ya kuhifadhi maji shambani kwa kilimo cha mvua na umwagiliaji 

 VIPIMO VYA KINGO ZA MAJARUBA

🌾Kingo kuzunguka shamba kimo  60cm-90cm na upana 30cm-60cm

🌾Matuta ya ndani (majaruba) kimo 40cm-50cm na upanda 30-50

 NAMNA YA KUTENGEZA JARUBA LA MPUNGA

🌾Weka alama kwenye mipaka ya jaruba kwa kutumia futi kamba, mambo na kamba ya mkonge.

🌾Kusafisha tabaka la juu la udongo na kuuweka katikati ya jaruba kwa kutumia jembe au chepeo

Chimba udongo wa tabaka la chini na kutumia kutengeza jaruba.

🌾Shindilia kingo na kusawazisha jaruba

🌾Ingiza maji kwenye jaruba kisha sawazisha jaruba kwa kuondoa udongo sehemu za miinuko na kuhamishia sehemu za mabondeni.

MBEGU ZA MPUNGA

🌾Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:


1️⃣Mbegu za asili za mpunga:

🌾 Mbegu za Asili Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo. Kuna aina nyingi za mpunga wa asili inayolimwa sehemu mbalimbali hapa nchini kama vile:⤵️

🌾Supa,Kahogo,Kula na Bwana,Shingo ya mwali,Saro,Wahi wahi n.k.


🌾Wakulima wanazipenda mbegu hizi kutokana na kuwa na sifa kama vile ladha nzuri, uvumilivu wa matatizo mbalimbali ya

kimazingira na kwa sababu ya uwezo wa mbegu hizi kustahimili katika hali mbaya ya hewa na hazihitaji uangalizi wa hali ya juu, Sifa hizi ni matokeo ya mbegu hizi kumudu mazingira na uchaguzi wa mbegu uliofanywa na wakulima kwa miaka mingi.Hata hivyo, mbegu nyingi  zinatoa mavuno kidogo, zinachelewa kukomaa, ni ndefu na rahisi kuanguka.


2️⃣Mbegu zilizoboreshwa{Mbegu za kisasa}:

🌾Hizi ni Mbegu zilizoboreshwa kutokana na mbegu za asili. Mfano

wa mbeguzilizoboreshwa ni kama vile:⤵️

🌾Katrin,IR54, IR64 , TXD88 ,TXD85,TXD306 {SARO 5} NERICA,SATO I, SATO II{Aina hizi mbili zinavumilia udongo wenye chumvi}

🌾 Tunawashauri wakulima waweze Kupanda mbegu zilizoboreshwa kwani huchukua muda mchache kukomaa na hutoa mazao mengi tofauti na Mbegu za Asili.

MAKUNDI YA MBEGU

🌾Kuna makundi ya aina tatu ya mbegu, ambayo ni mbegu ya muda mrefu mfano SUPA huchukua siku zaidi ya 140, mbegu za muda wa wastani mfano zile zote zilizoboreshwa ambazo huchukua siku  100-120 na kundi la mwisho ni mbegu za muda mfupi ambazo huchukua siku 90 hadi 100 mfano NERICA

 UCHAGUZI WA MBEGU

🌾Vitu vya kuangalia wakati wa uchaguzi wa mbegu

🌾Tabia ya mbegu {urefu na uchanuaji wake}

🌾Uzaaji wake

🌾Ukuaji wake{kuanzia upandaji hadi kuvuna}

🌾Mbegu vumilivu kwa udongo {Tindikali na alkalini}

🌾Mbegu kinzani kwa wadudu na magonjwa

🌾Ladha na ubora wa mchele.

 KUPIMA UWEZO WA MBEGU KUOTA ( GERMINATION TEST)

🌾Baada ya kuchagua aina ya mbegu utakayopanda chukua mbegu 100 na kuziweka kwenye kipande cha  gunia au kitambaa kilicholowanishwa maji. zifunike na kuzimwagilia maji kadri yanavyohitajika, siku ya nne hesabu mbegu zilizoota vizuri. Kama mbegu zilizoota ni  80  au zaidi mbegu hizo ni nzuri na zinafaa kupandwa kwenye kitalu au shambani .

Iwapo mbegu zilizoota ni kati ya 60 na 80 panda mbegu nyingi zaidi kwenye kitalu, yaani ongeza 20% hadi 40% na iwapo mbegu zilizoota ni chini ya 60 basi mbegu hizo hazifai kupandwa 

NB: Kwa mbegu zilizoota kati ya 60 na 80 panda kilo 24 hadi 42 kwa ekari

 UCHAGUZI WA  MBEGU KWA KUTUMIA MAJI, CHUMVI NA YAI{By salt-water floating method}.

🌾Vifaa vinavyohitajika kwaajili ya teknolojia hii ni:

↪️kilo1.5- 2kg za chumvi.

↪️Maji Lita kumi{10}

↪️Yai moja

↪️Ndoo mbili( ya lita 10 na lita 20

↪️Mbegu za mpunga

↪️Kijiti cha kukorogea.


 JINSI YA KUFANYA

🌾Changanya maji na chumvi kwenye ndoo ya lita 10

🌾Weka yai kwenye mchanganyiko wa maji na chumvi kama yai halitaelea ongeza chumvi mpaka lielee.

🌾Ondoa yai na weka mbegu za mpunga 5kg.

🌾Koroga kwa Kutumia kijiti na acha mbegu zitulie.

🌾Ondoa mbegu zitakazoelea,endelea kukoroga mpaka mbegu

zote nyepesi zinazoelea ziishe.

🌾Osha mbegu ambazo hazijaelea kwa maji safi mara 3 hadi 4  kuondoa chumvi.

🌾Ziloweke mbegu safi kwaajili ya kurahisisha

uotaji{pre-germination}.


 ZINGATIO

🌾Mbegu zitolewe kutoka kwenye maji na kusambazwa juu ya mkeka au gunia la mkonge lililowekwa juu ya kichanja ili maji yapate kuchuruzika baada ya hapo mbegu  zianikwe kivulini tayari kwa ajili ya kupanda kwenye shamba kavu au lenye unyevu wa wastani 

🌾Ukihitaji kupanda mbegu kwenye shamba lenye unyevu mwingi (tope) au kitaluni otesha mbegu kwanza kwa  kuziloweka  ndani ya maji  kwa saa 24  huku ukibadilisha maji  kila baada ya saa 12 ili kuzipa mbegu hewa baada ya hapo mbegu zitolewe kwenye maji kishahmara mbili huku akinyunyuzia maji endapo unyevu utapungua, mbegu zikichipua zifunuliwe na ni muda muafaka kupandwa kwenye udongo wenye unyevu kitaluni au shambani

Kuchanja mbegu

🌾Kabla ya kupanda Mbegu Kitaluni au shambani unashauriwa kuzichanja kwa kuzichanganya na Viuatilifu vyenye viambata vya Imidacloprid, Metalaxyl na Carbendazim.

▪️ Imidacloprid  Kiambata sumu hiki huikinga Mbegu isishambuliwe na Wadudu ikiwa Ardhini na hadi siku 40 kwa Vipepeo weupe{White Flies} ila kwa wadudu wengine ukiacha Vipepeo weupe puliza sumu zingine ili kuikinga Miche ya Mpunga baada ya kuota.

▪️Metalax na carbendazim viambata hivi huzikinga Mbegu zisishambuliwe na Magonjwa zikiwa Ardhini na hadi siku 40 baada ya kuota.

🌾Mfano wa Viuatilifu Ni Tunza Ina Kiambata Cha Imidacloprid pekee,Seed Plus au Seed Watch zina viambata vitatu ambavyo ni Imidacloprid, Metalax na Carbendazim kwa hio ukiipata sumu yenye Viambata vyenye Kukinga Mbegu isishambuliwe na Wadudu na Magonjwa ni Bora zaidi.

Muda wa Kuchanja mbegu

🌾 Kwa mkulima anaepanda Mbegu moja kwa moja Shambani, mbegu zinachanjwa mara baada ya kuosha kuondoa chumvi Kabla ya kuzianika kivulini na kwa mkulima anaepanda kwenye kitalu au shamba lenye tope mbegu zinachanjwa baada ya kuziloweka kwa saa 24 Kabla ya kuziotesha {Pre germited}.

KIASI CHA MBEGU

🌾Kwa ekari moja  mbegu za mpunga zinazohitajika ni kuanzia 20kg-30kg kama mkulima ataamua kusia mbegu moja kwa moja shambani na kilo 14 -18 kama mkulima ataamua kusia mbegu kitaluni.

UPANDAJI WA MBEGU ZA MPUNGA

🌾Kuna njia mbili kuu zinazotumika kupanda mpunga shambani Njia hizo ni ile ya:⤵️


▪️kupanda mbegu moja kwa moja shambani.

▪️kupandikiza miche shambani

 KUPANDA MBEGU MOJA KWA MOJA SHAMBANI

🌾Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu moja kwa moja kwenye shamba lililotayarishwa vizuri. 

1️⃣ Kumwaga Mbegu

🌾Hii ni njia ya kawaida waitumiayo wakulima kumwaga na kufukia mbegu (broadcasting).

2️⃣Kupanda mbegu kwenye mashimo yaliyo kwenye mstari na kwa kuzingatia nafasi maalumu.

3️⃣Kupanda mbegu kwenye mashimo bila kufuata mstari na bila kuzingatia nafasi iliyopendekezwa (dibbling). 

4️⃣Kupanda mbegu kwa kunyunyizwa kwenye vifereji yenye vina vifupi na kufukiwa pasipo kuwa na nafasi maalum kati ya punje na punje(seed drilling).

🌾 Tunawashauri wakulima watumie Njia mbili Kati ya nne tulizozitaja namba 2 na 4{Kupanda kwa nafasi maalumu na Kupanda kwa kutumia vifereji}.

🌾 Njia ya Kumwaga Mbegu hatushauri itumike kwani Njia hii hutumia mbegu nyingi, Mbegu hurundikana sehemu moja na Ni Vigumu kupalilia Kama utatumia zana{Push Weeder au Rotary Weeder}

KUOTESHA MBEGU KITALUNI

🌾Kitalu ni sehemu ya kuoteshea mbegu na kukuzia miche kabla ya kupandikiza shambani

 AINA ZA VITALU

🌾Kuna aina tatu za vitalu katika kilimo cha mpunga ambazo ni kitalu kikavu,dapog na kitalu tepetepe


1️⃣Kitalu kikavu

🌾Katika aina hii ya kitalu mbegu husiwa kwenye  udongo mkavu hufunikwa kwa udongo na humwagiwa maji ili ziote ,mbegu huchukua siku 4-7 kuota.

2️⃣Kitalu tepetepeù

🌾Mbegu zilizoatikwa {pre germinated} husambazwa vizuri kwenye kitalu na kisha hufunikwa kidogo kutumia udongo tifutifu, miche huchukua siku 2-3 kuchipua.

3️⃣Kitalu cha Dapog

🌾Mbegu huweza kuoteshwa sakafuni, juu ya karatasi za nailoni au hata juu ubao au meza, kitalu hiki huwekwa mahali popote na hutumika zaidi pale ambapo ni vigumu kusia mbegu shambani kwa mfano shamba kufurika maji au uvamizi wa panya na ndege Kwenye kitalu hiki mbegu zilizo atikwa {pre germinated} husambazwa juu ya sakafu au juu ya nailoni ambayo Inakuwa na Udongo kwa juu kisha hufunikwa na kiasi kidogo cha udongo tifutifu na kumwagiliwa maji mara yanapohitajika.

MAHALI PA KUWEKA KITALU

▪️Kitalu kikavu na kitalu tepetepe

🅰️Kitalu kiwekwe mahali ambapo⤵️

🌾Ni rahisi kumwagilia na kutoa maji yanayozidi

🌾Hakiwezi kuathiliwa na mafuriko

🌾Penye udogo wenye rutuba na hakuna kivuli

🌾Ni rahisi kusambaza miche ya mpunga wakati wa kupandikiza

🅱️Kitalu cha dapog

🌾Eneo linatakiwa la tambarare

🌾Kuna mwanga wa kutosha

🌾Maji ya kumwagilia yanapatikana kwa urahisi

🌾Ni rahis kufika na kusafirisha miche kwenda shamban

 UKUBWA WA KITALU

🌾Kitalu kinatakiwa kuwa na ukubwa wa  asilimia 5-10{5%-10%}ya eneo lote unalotaka kulima mpunga mfano eneo la ukubwa wa ekari moja(mita mraba 4000) kitalu kinatakiwa  kuanzia mita mraba 200 -400

🌾Asilimia 5 ya eneo la ekari moja ni mita za mraba 200.Kama utatengeneza kitalu cha urefu wa mita20 na upana wa mita 1, vitalu 10 vya ukubwa huu vinatosha kupandikiza eneo la ekari moja

 UTUNZAJI WA KITALU

🌾Kumwagilia

🌾Kupalilia

🌾Kudhibiti wadudu na magonjwa

🌾Uwekekaji wa mbolea:

 ▪️Kwa kitalu chenye ukubwa wa mita mraba 5 weka gramu 100 za mbolea za kupandia kama DAP,NPK

mita mraba 20 weka gramu 400 za mbolea za kupandia

 KUPANDIKIZA MICHE

🌾Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu kwanza kwenye kitalu

kabla ya kuzihamishia shambani.Mara Nyingi huchukua siku 21-30, kwa mbegu za muda mfupi ,siku 30-35 kwa mbegu za muda wa wastani na siku 35-40 kwa mbegu za muda mrefu,.Ili kupata mavuno mengi na kukifanya kilimo cha mpunga kuwa cha faida ni muhimu wakulima kuzingatia mbinu hii muhimu na kuachana na kilimo cha kiholela kwa kumwaga mbegu moja kwa moja shambani. Aidha kwa wakulima wanaofuata kanuni hii wamepata mafanikio makubwa.

 FAIDA ZINAZOPATIKANA KWA KUPANDIKIZA MICHE KITALUNI

🌾Mkulima huweza kuchagua miche bora na mizuri ikiwa

kitaluni.

🌾Miche hukua haraka na yenye afya .

🌾Kiasi kidogo cha mbegu huhitajika.

🌾Mavuno huwa mengi.

 SIFA ZA MICHE INAYOFAA KUPANDWA


🌾Mche uwe na majani matano{4-7} mafupi na yaliosimama.

🌾Shina la mche liwe imara.

🌾Majani ya mche yawe ya kijani.

🌾Mizizi ya mche iwe mengi na imara.

🌾Miche iwe na kimo kimoja.

🌾Miche isiwe na wadudu au magonjwa.

MAANDALIZI YA KUPANDIKIZA MICHE

🌾kumwagilia miche kwanza ili kupata urahisi wa kungo’a

🌾Ili kuzuia miche isikatike ovyo, miche ing’olewe kwa kushikwa chini  ya shina.

🌾Osha mizizi baada ya kung'oa na ondoa mabaki yote ya udongo.

🌾Epuka kung’oa miche mingi kwa wakati mmoja

🌾Usikate ama kupunguza majani wala mizizi ya miche.

🌾Miche ifungwe kwenye mafungu madogo madogo ili kurahisisha usafirishaji na upandikizaji shambani.

🌾Miche bora tu ndio ichaguliwe.

🌾weka miche iliong'olewa kwenye kivuli huku mizizi ikiwa kwenye  chombo chenye maji.

🌾Miche iliong'olewa isilazwe ipelekwe moja kwa moja Shambani kwa kwaajili ta kupandwa.

 JINSI YA KUPANDIKIZA MICHE

🌾Miche ishikwe kwa vidole vitatu wakati wa kupandikizwa.

Pandikiza kati ya miche 2 -3 kwa kila shimo{lakini inategemea na Aina ya Mbegu na Nafasi unayotumia}.

Kwa mafanikio zaidi, miche ipandikizwe katika kina cha sentimita 2-3.Ukipanda kina kirefu machipukizi huchelewa kujitokeza.Baada ya kupandikiza miche machipukizi hujitokeza baada ya siku 5-10

 NAFASI SAHIHI ZA KUPANDA MPUNGA

🌾Nafasi ya kupanda mpunga kwa mbegu bora ni:⤵️

15cm  kwa 15cm{15cm×15cm}.

20cm kwa sm 20cm {20cm×20cm}.

15cm kwa 30cm{15cm×30cm}.

10cm kwa 30cm{10cm×30cm}

20 kwa 20{20cm×20cm}

25 kwa 25 {25cmx25cm}

30 kwa 30{30cmx30cm}

🌾Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili {double rows}, nafasi kati ya mistari miwili ni sm 10, nafasi kati ya mmea na mmea katika kila mstari ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine{double rows} ni sm 40.

🌾Mbegu za asili zipandwe kwa nafasi ya:

•sm 20 kwa sm 20

•sm 25 kwa sm 25 

•sm 30 kwa sm 30.

Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo.

 USIMAMIZI WA MAJI KWENYE SHAMBA LA MPUNGA

🌾Kwanza shamba la mpunga linatakiwa liwe limesawazishwa

kabla ya kupanda miche.

🌾Mwagilia{Ingiza} maji kwenye shamba{majaruba} sentimita 1-3 baada ya kupandikiza miche kuzuia magugu.

🌾Wakati mpunga unatoa machipukizi ,yatoe maji yote kwenye majuruba kwaajili ya palizi na uwekaji wa mbolea Mara ya kwanza{1 top dressing}.

🌾Wiki tatu baada ya kupandikiza miche ingiza maji Shambani kimo cha sentimita 5-10.

🌾Wakati wa mpunga kutunga mimba{panicle initiation},kausha {yatoe} maji Shambani kwa siku moja kwaajili ya uwekaji wa mbolea awamu ya pili{2 top dressing},baada ya kuweka mbolea ingiza maji shambani kimo cha sentimita 10-15.

🌾Siku 10-21 kabla ya kuvuna mpunga kausha shamba kwa kuyatoa maji kwaajili ya kuruhusu ukomavu wa mpunga kwa pamoja na uvunaji.

NB; Ni bora na vizuri kuruhusu mzunguko wa maji Shambani ili kurahisisha uzungukaji wa hewa ya oxygen kwenye mizizi.

MATUMIZI YA MBOLEA KATIKA KILIMO CHA MPUNGA

🌾Mbolea ni chakula cha mimea, ambayo ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.

🌾Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu kama vile naitrojeni-N, fosfati-P na 

potashi-K. Madini mengine ni pamoja na salfa-S, chokaa-Ca (calcium), magnesium-Mg,Boroni-B, shaba-Cu, chuma-Fe, manganese, molybedenum na zinki-Zn. Haya madini kwa Asili, yanapatikana katika udongo kwa viwango tofauti. Yanapopungua 

kutokana na kilimo, inabidi yaongezwe kwa kutia mbolea.

 AINA ZA MBOLEA

🌾Kuna aina mbili za mbolea ambazo ni:

1.Mbolea za asili {organic fertilizers}

2.Mbolea za viwandani {inorganic or industrial fertilizers}

 1️⃣ MBOLEA ZA ASILI

🌾Mbolea za asili {organic fertilizers}.Hizi ni mbolea zinazotokana na wanyama na mimea. Mbolea za asili ni kama 

vile:⤵️

🌾Mbolea vunde{Compost Manure}.Mbolea hizi hutokana na mchanganyiko wa manyasi au mabaki ya mbao na samadi na majivu.

🌾Samadi{Farmyard Manure}.Hutokana na  kinyesi cha wanyama kama mifugo na ndege.

🌾Mbolea za kijani{Green Manure} Hutokana na kupanda mimea aina ya mikunde ambayo hukatuliwa na kuchanganywa na udongo.

🌾Majivu: ni mbolea ya asili yenye madini aina ya potashi kwa wingi, 

fosfati, chokaa na magnesium.

🌾Matandazo {mulches}: Matandazo yanayowekwa Shambani baadae huoza na huwa mbolea.

🕹️Mbolea za Asili huwekwa katika shamba la mpunga wakati wa kulima au Kuvunja vunja madogo makubwa{Pudding or Harrowing}.

UTENGENEZAJI WA MBOLEA VUNDE (MBOJI/COMPOSITE)

📝Mboji hutengenezwa kwa kukusanya mchanganyiko wa masalia ya mimea,samadi na 

majivu.Unaweza ukachimba shimo na kuweka mchanganyiko wako uvunde au unaweza ukachanganya mchanganyiko wako katika vyombo kama mapipa au mifuko migumu. 

 Kuna aina mbili za mboji

1⃣mboji ya kuanzia mwezi mitatu{3-6} na 

2⃣Mboji ya siku kumi 

na NNE{14}.

🌾Vitu na vifaa vinavyohitajika katika utengenezaji wa mboji ambayo ni:⤵

🌾Majani mengi mabichi/kijani na makavu. 

🌾Majani jamii ya mikunde ni mazuri sana kwani hutengeneza kirutubishi cha naitrojeni (N) kwa wingi,

🌾Mabua ya mahindi au vitawi vya miti,

🌾Udongo wa kawaida wa juu, 

🌾Samadi au mbolea yoyote ya wanyama au mboji ya zamani,

🌾Majivu au vumbi la mkaa na Maji

HATUA ZA UTENGENEZAJI WA MBOJI YA MWEZI 3-6    

🌾Chagua sehemu karibu na eneo ambalo mboji itaenda kutumika na ambapo kuna hifadhi ya kutosha kukinga dhidi ya upepo, jua na mvua. 

🌾Katakata majani yawe madogo madogo ili yaweze kuoza haraka.Tengeneza msingi kama mita sita (6) urefu na upana wake mita 2 kwa kutumia majani magumu kama matawi/vijiti. Hii itahakikisha maji yanatiririka na hewa ina zunguka vizuri.Hakikisha kuna nafasi ya kutosha kufanyia kazi kwenye biwi bila kulikanyaga. 

🌾Weka sentimita 10 ya majani ambayo hayaozi haraka kwa mfano mabua ya mahindi au mimea mibichi/kijani. 

🌾Weka sentimita 10 ya vifaa ambavyo huoza haraka kwa mfano maganda ya mboga na matunda.

🌾Weka sentimita 2 ya samadi (mbolea-hai ya wanyama),mabaki ya mbolea ya zamani kama yaweza kupatikana. 

🌾Weka udongo wa juu sentimita 10 kutoka kwenye shamba ambalo hulimwa. 

🌾Majivu na mkojo wa ng'ombe vyaweza kunyunyuziwa juu ili kufanya biwi/lundo kuoza Haraka. 

🌾Nyunyizia maji kwenye biwi mpaka lilowe. 

🌾Rudia mpangilio huu kuanzia namba nne (4) mpaka lundo lifike mita moja (1.m) hadi moja na nusu (1.5m) kwenda juu isipokuwa vijiti/matawi ya kwanza. 

 ZINGATIA

📝Biwi/lundo la mboji linatakiwa lifunukwe ili kupunguza/kuzuia mvuke ama mvua nyingi 

ambayo hubeba rotuba kutoka kwenye mbolea. Weka gunia, nyasi ama matawi ya ndizi yaliyokauka. 

📝Kila tabaka/kunjo/safu yafaa kupangwa kuanzia kwenye ukingo ili lundo la mbolea lisiporomoke. Namna nyigine ya kuzuia lundo kuporomoka ni kwa kuweka vipande vya mbao kando ya biwi. Wavu wa nyuzi za chuma utafanya biwi kukauka. 

 HATUA ZA UTENGENEZAJI MBOJI YA SIKU 14

🌾kusanya mimea, majani mabichi/kijani, samadi, maji, kijiti ambacho hakiozi haraka. 

🌾Katakata majani yawe madogo urefu wa sm 10 

🌾Changanya majani yaliokatwakatwa ,samadi na maji vizuri kwa uwiano wa 1:1:1,yani 

majani ndoo 1,samadi ndoo 1 na maji ndoo 1. 

🌾Chomeka mti katikati ya biwi. 

🌾Funika lundo/biwi kwa nyasi, gunia au majani yaliokauka. 

🌾Baada ya siku 3 pindua biwi sehemu ya juu iwe chini na ya juu chini iwe juu, pindua tena baada ya siku 4, pindua tena baada ya siku 4, pindua tena baada ya siku 3{jumla siku 14}.Kisha baada ya siku ya 14 mboji yako itakuwa tayari kwa matumizi.

ZINGATIA: Majani yatumike mabichi na ambayo hayajakomaa.

FAIDA ZA MBOLEA ZA ASILI

🌾Mbolea za asili hufanya kazi ya kuboresha hali ya udongo.

🌾 Huufanya udongo uwe na uwezo wa kuifadhi maji na hewa.

🌾Vilevile mbolea za asili hufanya udogo kuweza kutengeneza matundu mazuri ambayo husaidia mizizi ya mazao na hewa kupenya kwa urahisi.

2️⃣ MBOLEA ZA VIWANDANI

🌾 Mbolea za viwandani zimegawanyika katika makundi matatu, Mbolea za Kupandia, Mbolea za Kukuuzia na Mbolea za Kuzalishia.

🅰️Mbolea za kupandia {Basal fertilizer}. Hizi Mbolea zenye  kiwango  kikubwa cha Fosiforasi(P)

Hizi ni mbolea zinazowekwa katika shamba la mpunga wakati wa kuvunja vunja madogo makubwa{Pudding or Harrowing} au unaweza kuweka mbolea za  kupandia wiki moja  mpaka mbili baada ya mpunga kuota ,Mbolea hizi ni DAP,MINJINGU PHOSPHATE,MINJINGU MAZAO na NPK{yenye namba zinazofanana mfano 17:17:17 au yenye namba kubwa katikati mfano 10:15:10}  

🌾DAP:Ina virutubisho viwili{N=18% na P=46%}.

🌾NPK:Ina Virutubisho vitatu vya msingi mfano {N=17%,P=17% na K=17%}.

🌾Minjingu Phosphate:Ina Virutubisho viwili Fosfati{P2O5=29% na Ca=38% .  Chokaa inasaidia kukabili 

tindikali{Acidity} ya udongo.

🌾Minjingu Mazao: Mbolea hii inatokana na Minjingu Phosphate lakini imeongezwa

virutubisho vingineambavyo ni N={10%},Salfa {S=5%}, zinki{Zn=0.5%},Shaba{0.5%}, Boroni{B=0.1%}, pamoja na chokaa {25% CaO} na magnesium{1.5% MgO}. 

🕹️Mbolea za kupandia hasa Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao zinahitaji hali maalumu ya udongo ili ziweze kufanya kazi vizuri.Kwa mfano hali ya tindikali ya udongo inabidi iwe chini ya 6.2 ili mbolea za Minjingu ziyeyuke kwa kiwango cha kutosha. Kwa udongo wenye tindikali zaidi ya 6.2,tumia Mbolea ya DAP wakati wa kupanda.

🕹️Tumia Mbolea za Asili pamoja na mbolea za viwandani ili kuongeza mazao. 

🌾Mfuko 1 wa DAP unatosha eneo la ekari moja

🌾Mfuko 1.5 wa minjingu phosphate  na minjingu mazao mifuko 2 inatosha kwa ekari moja.

🌾Wakati ikihitajika kuweka virutubisho viwili au zaidi,na mbolea yenye virutubisho vyote vinavyohitajika haipo lakini mbolea zenye kirutubisho kimoja kimoja zipo unaweza kuzipima na kuzichanganya mbolea hizo kabla ya kuzitumia.Hata hivyo siyo mbolea zote zinazopatana zikichanganywa. Kwa mfano iwapo mbolea ya kupandia yenye N ni muhimu na unahitaji kuweka N na P wakati wa kupanda, usichanganye Ammonium sulfate-SA na Phosphate rock{mfano Minjingu} au Urea na Super-phosphate,Mbolea hizo zitajichanganya kikemikali na kusababisha kupungua kwa ufanisi.Ili kuwa salama zaidi ni vizuri kila mbolea itawanywe kwenye shamba pekee yake, mfano Minjingu kwanza 

kisha SA baadae.

🅱️Mbolea za kukuzia{Nitrogenous fertilizer( top dressing}.Hizi ni Mbolea zenye kiwango kikubwa cha nitrojeni(N)

🌾Hizi ni mbolea za  kukuzia zinazowekwa kwenye shamba la mpunga Mara mbili, Mara kwanza ni:

▪️Wakati machipukizi yanatokea{Tillaring phase}.

▪️Mara ya pili wakati maua yanaanza kutokeza{panicle initiations}au kabla ya kutunga mimba.Mbolea hizi huwekwa kwa njia ya kumwagwa{broadcasting}.

Mbolea hizi ni kama vile UREA,SA, CAN,Yara minner Winner na NPK (yenye namba kubwa mwanzoni mfano 15:10:10 au yenye namba zinazofanana mfano 17:17:17)

🌾Mfuko 1 wa UREA unatosha kwa eneo la ekari moja

🌾Mifuko 2 ya SA inatosha  kwa ekari moja

🌾Mifuko 2 ya mbolea ya CAN inatosha ekari moja.

↪️Kwa mbolea hizi zenye N weka angalau kwa vipindi viwili kwa viwango vilivyo sawa Mfano mfuko mmoja wa Urea wenye kilo 50 ambao unatosha kwa Ekari moja unaugawa, kilo 25 unaweka wakati Mimea inapacha na kilo 25 unaweka Awamu ya pili wakati suke linaanza kutungwa na kabla ya kuchanua.

🆎Mbolea za kuzalishia(NPK)

🌾Hizi ni mbolea zenye kiwango kikubwa cha patasium(K) ambazo huwekwa baada ya mpunga kutunga mimba mfano NPK  yenye namba kubwa mwishoni(10:10:20), tumia mfuko 1 hadi 2 ya mbolea hii kwa ekari moja

ANGALIZO

🌾Hakikisha wakati wa kuweka mbolea shamba la mpunga liwe limepaliliwa na liwe limeondolewa maji au kupunguzwa mpaka yafikie kimo cha Sentimita 3-5 ili kuhakikisha ufanisi wa Mbolea,Kama uliyatoa Maji yote Shambani baada ya kuweka Mbolea yaingize Maji haraka ili kuepusha upotevu wa N kwa kugeuka kuwa hewa.

🌾Usiweke Mbolea

wakati wa asubuhi sana au mara tu baada ya mvua kunyesha kwani kukiwa na hali ya Umande kwenye majani Mbolea zinaweza kunata kwenye majani na hivo kuweza kuunguza mimea.

KAZI YA VIRUTUBISHO VYA NPK NA DALILI ZA UPUNGUFU WAKE KWENYE MPUNGA

1️⃣FOSFETI{PHOSPHORUS}

KAZI ZAKE

🌾Husaidia uotaji mzuri wa mimea.

🌾Huimarisha mizizi,na hutumika katika utengenezaji wa chakula.

🌾Vile vile huhusika na usafirishaji wa nguvu kwenye mimea na hufanya mazao kukomaa haraka.

↪️UPUNGUFU WA FOSFETI {PHOSPHORUS}

🌾Dalili ya kwanza ni kupungua kwa kasi ya kukua na mashina kuwa membamba na upachaji unapungua.

Upungufu ukiwa mkubwa, mmea unakuwa na rangi ya zambarau.Rangi hii inaanzia pembeni mwa majani na kwenye mashina na baadaye husambaa kwenye jani lote. Rangi inaonekana vizuri zaidi upande wa chini wa jani.

🌾Majani ya mwanzo hukauka mapema na mizizi haikui vizuri kwenye mimea yenye upungufu kuliko ile yenye fosfati ya kutosha.

NITROGEN

Kazi yake⤵️

🌾Nitrogen huifanya mimea kukua haraka.

 🌾Nitrogen zinahusika na utengenezaji wa kijani kibichi kwenye mimea.

🌾Kutengeneza protini na kuupa mmea Afya bora

 ↪️UPUNGUFU WA NAITROJENI

🌾Mmea wa Mpunga unakuwa mdogo,mwembamba na hutoa suke dogo,na mwishowe hutoa mazao kidogo.Kama upungufu ni mkubwa sana mmea unaweza usitoe mpunga kabisa.

🌾Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mmea ambayo husababisha mmea kudumaa.

🌾Rangi ya kijani kwenye mmea hufifia na kugeuka taratibu kuelekea kwenye njano.Upungufu ukiwa mkubwa sana, majani hugeuka rangi ya njano Majani yaliyokomaa ndio huanza kugeuka.

🌾Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenye 

upungufu kuliko ile yenye naitrojeni ya kutosha.

POTASHI{POTASSIUM-K}

KAZI YAKE

🌾Husaidia mimea katika utengenezaji wa Protini na wanga.

🌾Huhusika na utumiaji wa madini muhimu kwa maisha ya mimea.

🌾Potash huwezesha Punje kukomaa na kuiva mapema lakini pia husaidia kutengeneza Punje bora.

🌾Potassium huimarisha Mimea na hupunguza uwezekano wa kuvunjika kutokana na Upepo au sababu zingine.

🌾Husaidia mimea kustahimili Magonjwa,Ukame, Baridi,na hali ya Udongo wenye Alkaline nyingi.

 UPUNGUFU WA POTASHI{POTASSIUM}

🌾Kupungua kasi ya ukuaji wa mimea,ambayo inasababisha mmea 

 kudumaa.

🌾Upungufu ukiwa mkubwa rangi ya kijani inafifia na mwisho 

kutoweka kabisa na sehemu iliyoathirika inakauka{necrosis}•Kutoweka kwa rangi ya kijani na kukauka kunaanzia pembeni mwa majani na kwenye ncha. 

🌾Majani yanakuwa na michirizi ya manjano na vinundu nundu kama migongo ya bati{yellowish streaks and corrugated}.

🌾Majani ya mwanzo hukauka mapema kwenye mimea yenye

upungufu kuliko ile yenye potashi ya kutosha.

↪️ Mpunga ukiwa na mapepe mengi wakati wa kuvuna jua kilichosababisha ni Upungufu au Ukosefu wa Potassium.

KUDHIBITI MAGUGU KATIKA SHAMBA LA MPUNGA{PALIZI}

🌾Magugu ni mimea inayoota mahali pasipo hitajika.Ushindani wa magugu na mimea hutegemea sehemu ambayo mpunga umepandwa,upandaji,aina ya kilimo cha mpunga na jinsi shamba lilivyoandaliwa na utunzaji kwa ujumla. 

MADHARA YA MAGUGU

🌾Hupunguza mavuno kutokana na kushindania virutubisho kutoka ardhini na kuathiri ubora wa mpunga 

🌾Huifadhi magonjwa na wadudu na hivyo kuongeza madhara yaletwayo na magonjwa na wadudu waharibifu kwenye zao la mpunga 

🌾Hupunguza ufanisi wa uvunaji wa mpunga kutokana na taka nyingi 

🌾Hupunguza ufanisi wa umwagiliaji kwa kuziba mifereji na kushindania na mpunga unyevunyevu uliopo mashambani.

↪️Kuna aina mbalimbali za magugu ya jamii ya nyasi na jamii ya majani 

mapana yanayosumbua sana katika kilimo cha mpunga hapa Tanzania. 

🌾Magugu muhimu zaidi katika kilimo cha mabondeni chenye kutegemea mvua na kile cha umwagiliaji ni punga pori.

PUNGA PORI {WILD RICE}

🌾Puga Pori {Wild Rice}limegawanyika katika makundi mawili ambayo ni punga punga{Oryza longistaminata} na Aina ya pili ni punga zeze{Oryza punctata} 

↪️Pungapunga-Linasambaa kwa njia ya mizizi na huishi kwa wakati wote na Pun8ga zeze-Linasambaa kwa njia ya mbegu na huishi kwa msimu.Mbegu hukaa ardhini kwa miaka mingi bila kuharibika

↪️Magugu hupunguza  mavuno kwa kati ya asilimia 11-45 kutegemeana na njia iliyotumika kuotesha mpunga. Mara nyingi magugu husumbua zaidi kwenye shamba lililopandwa mbegu moja kwa moja ukilinganisha na lile lililopandikizwa. Pia kuna usumbufu mdogo wa magugu katika shamba lililo na maji kuliko lile lisilo na maji{gongoni}.

Namna ya kudhibiti Punga pori 

🌾Andaa shamba{katua} mapema.

🌾Piga haro ili kulainisha udongo 

🌾Nyunyizia Viuagugu vya Glyphosate wiki mbili baada ya magugu kuota{Magugu yakiwa na Majani 3-4}. 

🌾Panda mbegu za mpunga 

🌾Nyunyizia kiua gugu Chaguzi mfano 2-4D wiki tatu baada ya mpunga kuota.

↪️Kuna njia nne{4} za Kudhibiti magugu katika shamba la mpunga

njia hizo ni⤵️:

🌾Kung'oa magugu kwa Kutumia mikono.

🌾Kuingiza maji shambani {Flooding}.

🌾Kwa Kutumia mashine {Rotary weeder na push weeder}.

🌾Kutumia kemikali{Herbicides} 

1️⃣ KUPALILIA KWA KUTUMIA MIKONO

🌾Njia hii ya kupalilia kwa kawaida ni kwa kutumia mikono lakini inawezakufanyika kwa kutumia jembe la mkono.

↪️Kuyang’oa magugu ni muhimu iwapo: 

🌾Kuyashughulikia magugu ya msimu na magugu mengine 

ya kudumu ambayo hayawezi kuota tena kwa kutumia mizizi au viazi vyake vya chini ya ardhi.

🌾Magugu yalioota kwenye shimo lililoota mpunga kiasi kwamba magugu hayo hayawezi kupaliliwa na zana za kupalilia.

2️⃣ KUPALILIA KWA KUTUMIA ZANA

🌾Kupalilia kwa kutumia zana kunafaa zaidi kwa miche iliyopandwa katika mistari iliyonyooka. Njia hii inatumia muda mfupi na gharama ndogo ya nguvukazi kuliko kwa kutumia mikono. 

🌾Njia hii kwa kawaida hufanyika kwa kutumia zana kama vile zile za kusukuma{Push Weeder} au za kuzunguuka{Rotary Weeder,inatumia Ingini}

Mambo ya kuzingatia wakati wa kutumia zana za kupalilia

🌾Hakikisha kuna unyevu wa kutosha kabla ya kupalilia.Inaweza kuwa ni vigumu kutumia zana za kupalilia iwapo 

udongo ni mkavu sana. 

🌾Pitisha zana ya kupalilia katikati ya mistari. Kwa kufanya 

hivyo, kufukia magugu na kukata mfumo wa mizizi na kusababisha magugu yafe kabla ya magugu mengine kuota tena. 

↪️Kupalilia kwa kutumia zana kunaweza kuwa 

na ufanisi mdogo kwani, magugu yaliyo katikati ya mistari hayawezi kupaliliwa. Ushindani wa magugu yatakayobaki utaathiri mimea ya mpunga.

3️⃣ KUPALILIA KWA KUTUMIA VIUAGUGU{HERBICIDES}

🌾Matumizi ya viuagugu ni moja ya teknolojia muhimu katika kudhibiti Magugu katika Shamba la Mpunga na hutumia nguvu kazi kidogo ukilinganisha na kutumia Njia ya mikono.

↪️Viuagugu vimegawanyika katika makundi yafuatayo:⤵️

🅰️Viuagugu vinavyoua magugu yote{Non Selective Herbicides}.

🌾Viuagugu visivyochagua Ni kama vile vyenye kiambato-amilifu aina ya glyphosate ambayo hutumika kabla ya kulima shamba la mpunga. 

↪️Mifano ya viuagugu visivyochagua ni Rondo,Force Up, Touchdown Forte,Round-up,Gugusate,Glyphocel,Gyraser,Paraquat,Gramoxone, n.k. 

🅱️Viuagugu vinavyowekwa kabla ya miche kuchipua

↪️Viuaugu hivi huwekwa kwenye udongo na huyadhibiti magugu kabla hayajachipua.

🆎Viuagugu vinavyochagua{Selective Herbicides} 

🌾Viuagugu hivi hupulizwa kuua magugu baada ya Mpunga kuota.

UDHIBITI WA MAGUGU KWENYE SHAMBA LA MPUNGA KWA KUTUMIA VIUAGUGU {SELECTIVE HERBICIDES}

1️⃣ VIUAGUGU VINAVYOPULIZWA KABLA MBEGU HAZIJAOTA{Pree Emergency Herbicides}

↪️Viuagugu hivi hudhibiti Magugu Kwenye Shamba la Mpunga na hupulizwa kwenye Shamba lililoandaliwa Vizuri siku 2-4 baada ya Kupanda mbegu na Kabla ya Magugu hayajaota.

↪️Mafano wa Viuagugu hivi Ni:⤵️

🌾Harness 900EC{Acetochlor 900g/L}

🌾Trek P EC{Terbuthylazine 270g/lt + Pendimethalin 64g/lt EC}

🌾Primagram Gold 660 SC{S-Metolachlor 290g/L+ Atrazine 370g/L}

↪️Stomp 455 CS{Pendimethalin 455g/l}

🌾Rilor 500EC{Pretilachlor 500g/l}

🌾Galaxy 16 WG=Pretilachlor 145g/Kg + Pyrazosulfuronethly 15g/Kg

🌾Sofit 300EC=Pretilachlor 300g/l.

↪️Viuatilifu hivi haviwezi kuziua Mbegu za Magugu bali zinachelewesha uotaji wake kwa miezi 2-4 kwa kutengeneza Utando{ Protective Layer} juu ya Udongo ambao hauwezi kuruhusu Mbegu za Magugu kuota na hata zikiota Magugu huuliwa tu pale zinapoanza kuota.Baada ya muda wa miezi 2-4 kupita Kemikali za Viuagugu huvunjwa{by Soil Microbes}

↪️Ili Viuagugu hivi viweze kufanya kazi vizuri puliza wakati Kuna Unyevu Shambani ili iweze kupenya Vizuri kwenye Udongo

2️⃣ VIUAGUGU VINAVYOPULIZWA BAADA YA MPUNGA KUOTA{Selective Herbicides}

A: Viuagugu vinavyoua Majani Mapana{Broad-leaved}

🌾2,4-D Amine

🌾Tiller Gold OD{164 

Isoxadifen-ethyl 75 g/l + Ethoxysulfuron 20 g/l +Fenoxaprop-P-ethyl 

69 g/l

B: Viuagugu vinavyoua Majani Mapana na Nyasi{Broad-leaved weeds and Grass}

 🌾Solito 320EC{Pretilachlor + Pyribenzoxim}

🌾Baraka 420EC=Propanil 360g/l + Triclopyr 60g/l 

🌾Bakapu 600EC=Thiobencarb 400g/l + Propanil 200g/l 

🌾Rilor 500EC=Pretilachlor 500g/L

🌾RipanilPlus 600 EC=Thiobencarb 400g/l +Propanil 200g/l 

🌾Rainbow 25 OD=Penoxsulam 25g/l

🌾Bebisy 30WP{Bispyribac-Sodium 18% +Bensulfuron-Methyl 12% 

🌾Penoxcy 160 OD{Cyhalofop–butyl 150g/L + Penoxsulam 10g/L }

🌾Beche Plus 300 WP=Bispyribac-sodium 180g/kg+Bensulfuron-methyl 120g/kg

C: Viuagugu vinavyoua majani Mapana na Jamii ya Ndago{Broad-leaved weeds and Sedges}

🌾Basagran 480 g/l=Bentazone 480g/l

🌾Agriforce 100 SC,Bispyribac-sodium 100g/l

🌾Vuna Rice 10SC{Bispyribac-Sodiu 100g/l}

D: Viuagugu vinavyoua Majani Mapana, Jamii ya Ndago na Nyasi{Broad-leaved Weeds,Sedges and Grass}

🌾 Rilor 500EC {Pretilachlor 500g/l}

🌾Stomp 455 CS{Pendimethalin 455g/}

🌾Basmati 550 SC=Pyriftalid 367g/l+Bensulfuron 183g/l 

🌾Falidox Xtra 180 WP=Fenoxaprop-p-ethyl 

100g/kg +Pyrazosulfuron 

80g/kg 

🌾Penoxcy 160 OD=Cyhalofop–butyl 150g/L + Penoxsulam 10g/L 

🌾Rainbow 25 OD=Penoxsulam 25g/l 

🌾Safuroni 715 WP=Quinclorac 48 %+ Pyrazosulfuron‐ethyl

1.5 % + Cyhalofop‐butyl 22% 

🌾Topshot 60 OD=Cyhalofop Butyl 

50g/L + Penoxculam 10g/L 

🌾Snowpanil 70% 

EC =Butachlor 35% +Propanil 35% 

 🌾Penox 110 OD=Penoxsulam 10g/L +Cyhalofop‐butyl100g/L 

Viuagugu vingine vinavyoua Magugu ya Aina Nyingi Ni ⤵️

🌾Nominee Gold=Bispyribac-Sodiu 100g/l

🌾RiceBack 400 SC{Bispiribac - sodium 400 g/l

🌾Kapunga Gold 

100SC=Bispyribac-sodium 100g/L

🌾Tripinil 600 EC=Thiobencarb 40% + Propanil 20% EC

🌾Hangzhou 

Hansunil 160 EC =Propanil 160 g/l

🌾Multi Rice Extra 30 OD=Penoxulam 50g/l +Cyhalofo-butyl 200g/l +Pyribezoxim 50g/l. 

↪️Multi Rice Plus 25 OD=Cyhalofo-butyl 20%+bispyribac-sodium 

5%. 

🌾Betazon 380 EC=Clomazone 240g/l + Pretilachlor 40g/l +Bensulfuronmethyl 100g/L 

🌾Kujehela Nil 600EC=Propanil 200g/L + Benthiocarb 400g/L 

🌾Basunil 600EC

=Propanil 200g/L+Thiobencarb 400g/L.

🌾Banstar 250EC=Oxidiazon 250g/L

🌾Ronstar 250EC=Oxidiazon 250g/L 

🌾Barof 395EC=Propanil 200g/L+Piperophos 195g/L

ZINGATIO

🌾Ni vema mkulima akaweza kuelewa aina ya magugu yaliyoko shambani mwake ndipo atafute mbinu ya kuyadhibiti kwa kutumia viua gugu, lini dawa itumike na kwa kiasi gani. 

🌾 Viuagugu hufanya Vizuri zaidi majani yakiwa machanga, Magugu yakiwa na Majani 1-5.

IMEANDALIWA na 

1️⃣ABUU  HAARITHA RAJAB MANDI-  0786945831

2️⃣BARAKA MHAGAMA(Agronomist)- 0719330046

Imehaririwa na kuchapishwa na;

Abbas Mpinga 0757- 139423 

kilimoforlife@gmail.com 


Maoni

Machapisho Maarufu