KILIMO BORA CHA ZAO LA KAROTI: carrots production

KILIMO BORA CHA KAROTI

Imeandikwa na Abuu Haarith +255 786 945 831
Imehaririwa na imefanyiwa marekebisho na Imechapishwa na Mr Mpinga (kilimo Expert)
 +255757139423
+255717439423


UTANGULIZI
Karoti ni zao la mizizi ambalo hulimwa zaidi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mbeya na Kagera.
Zao hili hutumika kama kiungo katika mapishi ya vyakula mbalimbali. Huweza kutafunwa mbichi au kuchanganywa kwenye kachumbari.

Karoti zina vitamin A, C na madini aina ya chuma.

  MAZINGIRA/HALI YA HEWA :
Karoti hustawi vizuri kwenye sehemu zenye joto la wastani (nyuzi joto 15 hadi 27 za Sentigredi).

Kiasi cha mavuno yanayoweza kupatikana na ubora wa karoti, hutegemea sana aina ya udongo. Hivyo karoti hustawi vizuri katika udongo mwepesi, wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu na usiotuamisha maji.

  AINA ZA KAROTI
Kuna aina nyingi za karoti. Zifuatazo ni aina zinazolimwa hapa Tanzania.

Nantes
Karoti za Nantes ni ndefu, huvunjika kwa urahisi, zina umbo la kuchongoka na ncha kali. Aina hii hupendwa sana kutafunwa na walaji, kutokana na ladha yake tamu. Karoti za Nantes hazifai kwa kusindikwa.

Chantenay Red Core
Hizi ni nene kwa umbo, na zenye ncha butu. Unene wa nyama ya nje na ndani hulingana hivyo zinafaa sana kwa kusindikwa. Huwa na rangi ya machungwa iliyofifia na ladha yake siyo tamu.Aina hii hustawi vizuri kwenye udongo mzito.

Oxheart
Karoti za Oxheart ni fupi na nene. Huvunwa baada ya muda mfupi kulinganisha na aina zingine.

Cape Market
Aina hii hupendwa sana kutafunwa zikiwa mbichi pia zinafaa kusindikwa.

Flacoro
Aina hii huzaa sana na mizizi yake ni mirefu. Hufaa kwa kuhifadhiwa na kusafirishwa, kwa sababu haziharibiki haraka.

Top Weight
Aina hii ina sifa kama za Flacoro.

  KUTAYARISHA SHAMBA
Ili kupata mavuno mengi na bora, eneo la kupanda halina budi kutayarishwa vizuri. Iwapo shamba ni jipya, miti na visiki vyote vikatwe. Visiki na takataka zote ziondolewe shambani. Baada ya hapo shamba lilimwe vizuri na katika kina cha kutosha. Lainisha udongo ili kurahisisha uotaji wa mbegu za karoti ambazo ni ndogo sana. 
Kama eneo lina udongo wa mfinyanzi au wa kichanga ni muhimu kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. 
Mbolea hizi hufanya udongo wa mfinyazi uwe mwepesi wa kuweza kuruhusu maji na hewa kupenya kwa urahisi.
Endapo karoti zitastawishwa wakati wa mvua nyingi zipandwe kwenye matuta yaliyoinuliwa.


  KUPANDA

Karoti hupandwa moja kwa moja shambani katika matuta au sesa. Kiasi cha gramu 80 (sawa na vijiko vidogo vya chai 16) kinatosha kupanda eneo la mita mraba 100. Hekta moja huhitaji kilo 8 za mbegu na Ekari moja mbegu kilo 2- 3.
Hakikisha mbegu unazozipanda zina uwezo wa kuota kwa kuzifikicha. 
Mbegu zenye uwezo wa kuota hutoa harufu kali unapozifikicha. 
Zilizopoteza uwezo wa kuota huwa hazitoi harufu yoyote. Ili mbegu ziote haraka ziloweke katika maji kwa muda wa saa 24. 
Baadaya hapo changanya mbegu hizo na mchanga, kwa uwiano saww ili kupata mchanganyiko mzuri wa mbegu wakati wa kupanda. 
Kama utapanda karoti katika matuta, tengeneza matuta yaliyoinuliwa kidogo, kiasi cha sentimita 10 mpaka 15.
Matuta haya yawe na upana wa sentimita 60 na urefu wowote. Sia mbegu katika mistari yenye nafasi ya sentimita 30 mpaka 40 kati ya mstari na mstari, na kina cha sentimita moja mpaka moja na nusu. 
Iwapo utapanda katika sesa tumia nafasi ya sentimita 40 mpaka 50, kati ya mstari na mstari.
Nafasi ya kupandia itategemea aina ya karoti inayokusudiwa kustawishwa Baada ya kupanda, weka matandazo kama vile majani makavu na kisha mwagilia maji asubuhi na jioni mpaka mbegu zitakapoota.

Kwa mashamba makubwa ni vigumu kukadiria nafasi baina ya mistari na wala kuweka matandazo. Hivyo mbegu hutawanywa kwa kumwagwa bila mpangilio (Broadcasting).
Mbegu huota baada ya siku 10 mpaka 15. Zikishaota ondoa matandazo.

  UMWAGILIAJI
Umwagiliaji utategemea hali ya hewa. Mwagilia shamba la karoti pindi tu udongo utapohitajia maji, Shamba lisikae muda mrefu bila maji.


  KUTUNZA SHAMBA
Hakikisha udongo una unyevu wa kutosha hasa siku za mwanzo.
Karoti zikizokosa maji kwa muda mrefu huzaa mizizi midogomidogo.
Pia udongo mkavu ukipata maji mengi ghafla husababisha karoti kupasuka. 
Hivyo mwagilia shamba mara kwa mara kuhakikisha udongo una unyevu wa kutosha wakati wote, kama hali ya hewa ni ya jua kali.

  KUPUNGUZA MICHE
Mimea ya karoti inahitaji kupunguzwa mara mbili. Mara ya kwanza hupunguzwa ikiwa na majani matatu mpaka manne au wiki mbili tangu kupandwa na kuachwa katika nafasi ya sentimita tano mpaka saba. Mara ya pili hupunguzwa ikiwa na urefu wa sentimita 10 mpaka 13, na kuachwa katika nafasi ya sentimita 10 mpaka 15 baina ya mche na mche.
Karoti zilizopunguzwa zinaweza kutumika kwa chakula.

  PALIZI
Zao la karoti linahitaji kupaliliwa mara kwa mara. Palilia kwa kupandishia udongo na kuwa mwangalifu ili usikate au kudhuru mizizi.

 MBOLEA
Weka mbolea ya chumvichumvi aina ya DAP siku 7 baada ya karoti  kuota.
Weka mbolea ya S/A kama mbolea za asili hazikutumika wakati wa kupanda. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 100 kwa hekta. Weka kilo 50 kwa hekta iwapo mbolea za asili zimetumika. Mbolea iwekwe wakati wa kupunguza miche mara ya pili. Weka katikati ya mistari na kwenye mifereji na kisha fukia.

 Kuzuia Magonjwa na Wadudu Waharibifu:

Magonjwa:

Madoajani (Leaf Spot)
Ugonjwa huu husababishwa na kuvu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15.
Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano.
Ugonjwa ukizidi majani hukauka.

Kudhibiti
Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia viuakuvu kama vile.
Dithane-M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil Gold.

Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot).
Ugonjwa huu husababishwa na kuvu (Sclerotinia sclerotiorum)  na hushambulia mizizi na majani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.

Kudhibiti
Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
Nyunyuzia viuwaku kama vile Dithane M- 45, Blitox, Topsin - M 70% na Ridomil.

Wadudu
Minyoo Fundo (nematodes)


Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao ya jamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unaweza kupanda mazao ambayo hayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi.
Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.

  Karoti Kuwa na mizizi Mingi (Folking)

Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi, mawe na usiolainishika vizuri.
Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi.
Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.

  KUVUNA
Karoti huwa tayari kwa kuvunwa baada ya wiki 10 hadi 12 tangu kupandwa kutegemea hali ya hewa. Wastani wa mavuno kwa hekta moja ni tani 25 au zaidi.

KUTUNZA
Karoti huhifadhiwa katika mojokofu na asilimia kubwa ya wakulima hawana vihifadhisho vya zao la karoti. 
Hivyo karoti hujihifadhi yenyewe kwa mfumo wake wa asili 
Karoti inaweza kukaa hadi wiki bila kuharibika katika mazingira ya joto ridi la wastani 25 ⁰C.

MASOKO
Soko kubwa la karoti ni kupitia masoko ya kawaida katika miji. Na karoti inaweza kuachwa shambani muda mrefu shambani bila kuvunwa ili kusubiri soko litengamae.

MWISHO 

Wasiliana nasi 
+255757139423
+255717439423

Maoni

Machapisho Maarufu